KIONGERA NDIO BYE BYE SIMBA
Raphael Kiongera,
HATIMAYE mshambuliaji wa Simba, Mkenya Raphael Kiongera, juzi Jumanne jioni aliondoka nchini kwenda India kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji wa goti huku akisema atakuwa tayari kwa uamuzi wowote utakaotolewa na viongozi wake, kikubwa anachowaza sasa ni tiba na atarudi uwanjani atakapoona yupo fiti.
Kiongera aliumia goti la mguu wa kulia katika mechi yao ya kwanza ya Ligi Kuu Bara msimu huu dhidi ya Coastal Union na kumlazimu kukaa nje ya uwanja kwa miezi miwili ingawa sasa alianza mazoezi mepesi.
Mchezaji huyo ataenguliwa jina lake kwenye usajili mdogo unaoendelea ambapo tayari nafasi yake imechukuliwa na Mganda Dan Sserunkuma huku yeye atarejea Simba msimu ujao baada ya kupona kabisa kwani akifanyiwa upasuaji atalazimika kucheza mechi za ushindani kuanzia Februari au Machi mwakani wakati huo ligi ikienda ukingoni.
Kiongera aliliambia Mwanaspoti kuwa anaamini viongozi wake wanamjali na ndio maana wameamua kumtibu jambo ambalo kwake ndiyo kubwa kwa sasa kwani hawezi kucheza akiwa na majeruhi. Amesema endapo wataamua kumwacha, hatakuwa na sababu ya kung’ang’ania.
“Unajua mimi ni mchezaji, nimekaa nje muda mrefu lakini nashukuru viongozi wangu wameamua kunitibu kwa kunipeleka nje kufanyiwa upasuaji, hilo tu wameonyesha kujali na ndilo jambo kubwa ambalo nahitaji kwa sasa,” alisema.
“Sijaambiwa jambo lolote kuhusu kuachwa ama kubaki Simba, ila nimesikia wamemsajili Sserunkuma ambaye ni mchezaji mzuri pia na hawatajutia kumsajili straika huyo, hivyo siwezi kuzungumzia zaidi juu ya hilo, lakini yatakapotokea nitakubaliana nayo.”
Kwa upande wake, Kocha wa Simba, Patrick Phiri alisema: “Kiongera si mchezaji mbaya, ila tatizo ni hayo majeraha, ndiyo maana nililazimika kutafuta mbadala wakae haraka kwani nitamkosa katika mechi nyingi zijazo, naamini akipona viongozi watamrudisha kwani ni jambo ambalo hata yeye anatakiwa kukubaliana nalo.”
Comments
Post a Comment