WATOTO WACHOMWA MOTO NA KUFA KISA HAWARA
INASIKITISHA sana! Vijana wawili, Jumanne Omar (17) na Mgeni Rashidi Rajabu (16) (aliyekuwa mwanafunzi wa kidato cha nne Shule ya Sekondari Keko), Dar, wakazi wa Mtoni Madafu, Temeke wameuawa kwa kuchomwa moto na wananchi wenye hasira kali baada ya kudhaniwa kuwa ni wezi.
Tukio hilo la kinyama lilitokea wiki iliyopita Gongo la Mboto, Dar ambapo kijana aliyefahamika kwa jina la Hassan ambaye ndiye mkazi wa huko alidaiwa kuwafuata marehemu hao Mtoni Madafu na kuwaambia ametumwa na mama yake mzazi aende akafanye vurugu kwa hawara ‘mchepuko’ wa baba yake.
Inadaiwa kuwa, Hassan akiwa na vijana wengine wawili, aliongozana na vijana hao kwenda Gongo la Mboto kwa mwanamke huyo ambaye ni mama lishe.Ndugu mmoja wa Jumanne anasimulia: “Walipofika kwa mama lishe huyo ambaye Hassan alidai ndiye mchepuko wa baba yake, waliagiza chakula. Walipomaliza kula yule mama aliwadai pesa, Hassan akasema hawana na hawatoi.
“Tunasikia yule mama akaamua kukusanya vyombo walivyolia chakula ili akaoshe, lakini ghafla Hassan alimpora simu na pesa za mauzo na kukimbia na wale wenzake wawili ambao ni wakazi wa hukohuko Gongo la Mboto na kuwaacha Jumanne na Mgeni.
“Ilibidi mama lishe apige kelele za mwizi, watu wakatokea na kumkamata Mgeni na kuanza kumpiga, baadaye wakamkata kisogoni kwa panga huku Jumanne akikimbia kuomba msaada na kujitetea kuwa wao si wezi naye akakamatwa na kuanza kupigwa.
“Wakati wananchi hao wakiendelea kuwapiga vijana hao, alitokea dereva wa bodaboda ambaye alishauri kuwa vijana hao wachomwe moto mpaka wateketee.“Alikwenda kuchukua petroli na kuja kuwamwagia kisha akawasha kiberiti na vijana wakaanza kuungua moto huku wakipiga kelele kuomba msaada.”
Ilidaiwa kuwa, baada ya kupata taarifa hizo ndugu walizunguka kutafuta miili ya vijana hao na kuikuta katika Kituo cha Polisi cha Stakishari, Ukonga, Dar na baadaye kupelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya uchunguzi kabla ya mazishi.
Dada wa Jumanne anasimulia: “Sisi tulipigiwa simu na mpangaji mwenzetu saa mbili usiku, yeye anafanya shughuli zake hukohuko Gongo la Mboto, akatuambia mdogo wetu anauawa kwa kuchomwa moto, tukashangaa sana na kujiuliza imekuwaje na nini kimempata.
“Tuliondoka hapa na kuanza kupita kwenye hospitali kubwa tukianzia Temeke, Mwananyamala mpaka Muhimbili hatukukuta mwili, tukaamua kwenda Polisi Stakishari ndiyo tukakuta miili ya wawili. Inauma sana jamani mimi mpaka leo hii siamini.”
Naye baba mzazi wa Mgeni, Rashid Rajabu ambaye anaishi Zanzibar alisema:
“Kifo cha mwanangu kimeniumiza sana. Nakumbuka siku si nyingi nimetoka kumlipia ada ya mwaka mzima shuleni kwa sababu ilikuwa amalize kidato cha nne mwaka huu.
“Kifo cha mwanangu kimeniumiza sana. Nakumbuka siku si nyingi nimetoka kumlipia ada ya mwaka mzima shuleni kwa sababu ilikuwa amalize kidato cha nne mwaka huu.
“Naamini yote ni mipango ya Mungu japo mwanangu alikuwa kichwa darasani hata wanafunzi wenzake wameumia lakini hawanifikii mimi mzazi. Ngoja tuwaachie wahusika maana nimesikia suala hili limeshafika polisi,” alisema baba huyo.Miili ya vijana hao ambao iliharibika kwa moto, ilizikwa katika Makaburi ya Mtoni kwa Kombo, Jumatatu ya Aprili 13, mwaka huu.
Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi. Amina.
Uwazi linaendelea kufuatilia sakata hili kwa kina ili kujua nini kilitokea kwa Hassan, yupo wapi na mama lishe alichukuliwa hatua gani.
Uwazi linaendelea kufuatilia sakata hili kwa kina ili kujua nini kilitokea kwa Hassan, yupo wapi na mama lishe alichukuliwa hatua gani.
Comments
Post a Comment