RONALDO AKASIRISHWA NA SWALI LA RAMOS, AONDOKA



NEW YORK, MAREKANI
DAWA ya jeuri kiburi. Usimuulize Cristiano Ronaldo swali analoliona la kijinga, ataondoka zake. Ndicho kilichotokea juzi Jumapili baada ya kuulizwa kama Sergio Ramos ataondoka Santiago Bernabeu au hataondoka.
Ramos amekerwa na hali ya mkataba wake Santiago Bernabeu na inadaiwa kuwa ameipa timu hiyo mpaka Ijumaa wiki hii kutatua suala la mkataba huo kabla ya Real haijatimkia katika ziara yake katika nchi za Australia na China.
Inadaiwa kuwa wiki iliyopita United ilitoswa katika dau lake la Pauni 35 milioni na Real Madrid kwa ajili ya staa huyo wa kimataifa wa Hispania ambaye anaamini kuwa Madrid imeweka pesa kiduchu katika mkataba wao mpya.
“Sijui. Sijui,” Alisema Ronaldo huku akionekana kukasirishwa na swali hilo na kuamua kuvua vipaza sauti na kuondoka studio.  Lakini kabla hajaondoka, Ronaldo alikiri kwamba hana matatizo na kocha mpya wa klabu hiyo, Rafa Benitez na kudai kwamba atafanya naye kazi vizuri.
“Sijawahi kufanya kazi na yeye, lakini ni kocha mwenye uzoefu mkubwa. Tuone kitakachotokea. Real Madrid ni klabu kubwa duniani. Siku zote inatoa changamoto kwa wachezaji na makocha,” alisema staa huyo wa kimataifa wa Ureno.
“Ningependa kufanya kazi na yeye. Tuone kama tunaweza kushinda mataji muhimu. Nina uhakika na hilo.”
Hata hivyo, ni uhamisho wa Ramos ndiyo ambao unaonekana kuzua kizaazaa nchini Hispania na barani Ulaya kwa jumla. Juzi, staa wa Barcelona, Andres Iniesta ambaye timu yake ina upinzani wa kufa na Real Madrid alikiri kwamba haoni kama mchezaji huyo anaweza kuruhusiwa kuondoka.
“Siku zote nimesema kuwa Sergio ni mmoja kati ya mabeki bora wa kati duniani. Tayari yupo katika timu kubwa, lakini kusema kweli sioni Madrid wakimruhusu kuondoka,” alisema Iniesta.
Mmoja kati ya wachambuzi mahiri wa soka la Hispania, Graham Hunter,  alidai kwamba anadhani dili la mchezaji huyo kwenda Manchester United litafanikiwa kwa sababu mwenyewe ameomba kuhama.
“Ramos ameimbia Madrid moja kwa moja kwamba anataka kuondoka katika kipindi hiki cha majira ya joto. Amewataka waanze mazungumzo na Manchester United na hataki Real iongee na timu yoyote zaidi ya Manchester United,” alisema Hunter.


Hata hivyo, beki wa zamani wa Manchester United, Rio Ferdinand ambaye ameachana na soka, amedai kwamba haoni kama Ramos atakwenda Old Trafford.

Comments

Popular posts from this blog

JINSI YA KUKAA NA NGUVU ZA MUNGU SEHEMU YA KWANZA