MAGUFULI ATAMBULISHWA ZANZIBAR, AAHIDI KUFUATA NYAYO ZA KARUME NA NYERERE
MGOMBEA
urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amesema endapo
akifanikiwa kuchaguliwa kuwa rais wa Tanzania, ataongoza nchi kwa
kufuata nyayo za waasisi wa Taifa, Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius
Nyerere na Abeid Amani Karume.
Dk.
Magufuli alitoa kauli hiyo mjini Unguja, Zanzibar jana, baada kupokewa
na mamia ya wananchi kwenye Uwanja wa Ndege wa Karume, huku akiwa na
ulinzi mkali tofauti na siku zote.
Alisema viongozi hao waliweka misingi iliyojali kila mtu jambo ambalo limesaidia kuweka umoja, amani, utulivu na mshikamano.
“Nawahakikishia kuwa nitafuata nyayo za waasisi wetu endapo mtanipa ridhaa ya kuongoza Oktoba, mwaka huu.
“Nina
deni kubwa kwenu na kwa nchi yangu, eleweni hamtajutia uamuzi wa
kunichagua, nitafanya kazi kwa bidii, utii na maarifa kulijenga Taifa
hili bila kumbagua mtu yeyote,” alisema Dk. Magufuli
Alisema
Taifa lolote duniani linalopuuzia kujenga umoja, upendo na mshikanao wa
kitaifa, hupoteza haiba na dhamira ya kujenga uchumi imara.
Dk.
Magufuli ambaye aliambatana na mgombea mwenza wake, Samia Suluhu
Hassan, alisema atatimiza kile ambacho Watanzania wanakitegemea kutoka
kwake.
“Nataka
niseme jambo muhimu kwa Watanzania wenzangu, sikuja hapa kwa ajili ya
kampeni, tambueni bila umoja, amani na utulivu hakutakuwa na mageuzi
yoyote au mikakati ya kupambana na kutokomeza maadui ujinga, umasikini
na maradhi,” alisemas Dk. Magufuli.
Alisema ataongozwa na ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/20 ili kuhakikisha sekta ya utalii Zanzibar inakua.
Kwa
upande wake, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk.
Ali Mohamed Shein, alisema anamfahamu Dk. Magufuli kuanzia mwaka 1996,
akimtambua kuwa ni kiongozi mchapakazi mahiri, hodari na mzalendo.
Alisema kuteuliwa kwake ni kielelezo kinachothibitisha kukubalika kwa mgombea huyo ndani ya chama chake.
Kwa
upande wake, Samia aliwasifu wanawake wenzake wawili walioingia tano
bora na baadaye tatu bora; Balozi Amina Salum Ali na Dk. Asha-Rose
Migiro kwa kusema ushupavu wao na umadhubuti wamewatia ari na moyo
wanawake wengine nchini.
Mapokezi
hayo yalihudhuriwa na Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali
Idd, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Pandu Ameir Kificho,
Waziri Kiongozi mstaafu, Shamsi Vuai Nahodha, manaibu katibu wakuu wa
CCM Zanzibar na Bara, Vuai Ali Vuai na Radjab Luhavi, Mwenyekiti wa CCM
Mkoa wa Mjini Unguja, Borafya Silima Juma na baadhi ya mawaziri.
Comments
Post a Comment