MAVUGO AWATOA HOFU SIMBA



STRAIKA mpya wa Simba, Laudit Mavugo, amefunguka na kusema kuwa mechi ya upinzani kati ya timu yake ya Vital’O na Inter Stars ndiyo inayomzuia kujiunga mapema na timu hiyo na kuwatoa hofu mashabiki kwamba anakuja wiki ijayo.
Mechi hiyo ambayo ni ya nusu fainali ya Kombe la FA, itachezwa Jumamosi hii ambapo kwa nchi ya Burundi ni kama mechi ya Simba na Yanga zinapocheza nchini Tanzania.
Mavugo aliliambia Mwanaspoti kuwa viongozi wake wamemuomba awepo katika mechi hiyo hivyo kwake hakuna tatizo kwani akimaliza mechi hiyo tu ndipo atajiunga na Simba.
“Mimi sina tatizo lolote kujiunga Simba na nafikiri baada ya mechi yetu na Inter Stars nitakuja, ni mechi muhimu sana ambayo tunatakiwa tushinde kwa huku ni watani halafu ni nusu fainali ya Kombe la FA.
“Nafurahi kusikia Simba wameingia kambini mapema, kuchelewa kwangu si tatizo kwani huku naendelea na mazoezi kama kawaida ila maandalizi ya mapema yatasaidia sana kufanya vizuri kwenye ligi, tukicheza mechi tu ndipo nitakuja,” alisema Mavugo.
Mavugo ambaye amefunga mabao 34 kwenye Ligi Kuu Burundi, alifunguka kwamba msimamo wake wa kutua Simba upo pale pale ingawa alisisitiza kwamba endapo viongozi wa Simba hawajamalizana na klabu yake basi wafanye haraka kuhakikisha wanamalizana ili asipate pingamizi ambapo tayari imeelezwa kwamba Simba wameishamalizana na Vital’O.
“Nina makataba wa mwaka mmoja, kuna pesa fulani viongozi wangu walitaka wapewe na Simba, nafikiri wametatua hilo, mimi nilishamalizana na Simba,” alisema Mavugo.
Mavugo alikuwa mchezaji wa kwanza wa kigeni kusajiliwa Simba kwa ajili ya msimu ujao akifuatiwa na beki Emery Miboma anayetokea pia Vital’O na kumalizia na Hamis Kiiza kutoka Uganda.
Tayari Simba ina wachezaji sita wa kigeni wakiwamo Emmanuel Okwi, Simon Sserunkuma na Juuko Murshid ambao wote ni raia wa Uganda.
 Simba itafunga idadi ya wachezaji saba wa kigeni kwa kumsajili mchezaji kutoka Brazil.
Timu hiyo iliingia kambini juzi Jumatatu wilayani Lushoto Tanga bila makipa Hussein Sharif ‘Casillas’ aliyeomba ruhusa, Ivo Mapunda’ Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ ambao ni majeruhi. Wengine ni Jonas Mkude, Hassan Isihaka, Ramadhan Singano ‘Messi’ na Said Ndemla ambao watajiunga na kambi hiyo muda wowote.

Comments

Popular posts from this blog

JINSI YA KUKAA NA NGUVU ZA MUNGU SEHEMU YA KWANZA