KOTI LA WASIRA: KAMBI YA MEMBE LAWAMANI



Tukio la takribani wiki mbili zilizopita lililofanywa na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wassira,(pichani) la kukosea kufunga vifungo vya koti lake katika mkutano wa Injili wa dhehebu la Wasabato uliofanyika Februari 7, mwaka huu, limeipa lawama kambi ya kusaka urais inayoongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernand Membe. 
 
Wafuasi wa Waziri Wassira, ambaye kama Membe, naye ametangaza nia yake ya kuwania kuteuliwa na CCM ili kupeperusha bendera yake katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu, wanaamini maofisa wa Wizara ya Membe, waliisambaza picha hiyo makusudi, kwani walikuwa na picha zingine zilizopigwa baada ya kuwa amerekebisha uvaaji wake.
 
“Ni kweli kipindi cha mwanzo sikuweka vizuri vifungo vya koti langu, ila baada ya kuambiwa hilo na mzee Kuboja nililiweka sawa, sasa nashangaa ofisi ya huyo jamaa yangu inasambaza picha ya awali ili tu kunidhalilisha. Kwa kweli nimehuzunika sana, nimefadhaika sana, na nimejua kwamba hizi mbio za urais wengine wanazitumia kama nafasi ya kuwachafua wenzao,” alinukuliwa Wassira akisema, mara tu baada ya picha hizo kuanza kuonekana katika mitandao ya kijamii.
 
Wafuasi wake ambao wanaamini kuvuja kwa picha hiyo kumemharibia katika harakati zake, walisema kambi ya Membe ina hofu na nguvu za mtu wao, ndiyo maana wametumia fursa hiyo kumdhalilisha.
 
“Hapa hatumlaumu Waziri Membe, inawezekana kabisa yeye hahusiki na hajui lolote, ila kwa vyovyote hawa ni wapambe wake ambao huenda wanamuona Wassira kama tishio kwa mtu wao, wanaamua kufanya hivi wakiamini itasaidia kumshusha, hamna kitu,” alisema mpambe mmoja aliyekataa kutaja jina lake, kwa kile alichodai kulinda masilahi yake.
 
Wakati muda wa kuanza kwa hatua za uteuzi ukiwa unakaribia, vita kubwa inaendelea ndani ya CCM baina ya watu mbalimbali waliotangaza nia ya kuwania nafasi hiyo kwa lengo la kumrithi Rais Jakaya Kikwete anayemaliza kipindi chake cha miaka kumi mwaka huu. Vita hivyo vinaambatana na kuchafuana kwa namna mbalimbali, ikiwemo uzushi, kejeli na kashfa.
 
Tukio la Waziri Wassira lilitokea siku hiyo wakati wa zoezi la kupiga picha ya pamoja na kiongozi wa dhehebu la Wasabato duniani ambaye alikuwa nchini katika ziara rasmi.

Comments

Popular posts from this blog

JINSI YA KUKAA NA NGUVU ZA MUNGU SEHEMU YA KWANZA