JANUARY MAKAMBA: NIKISHINDWA URAIS NITARUDI JIMBONI KUGOMBEA UBUNGE
NAIBU Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, amesema kuwa akishindwa katika mchakato wa kura za maoni za kusaka urais ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), atarudi jimboni kuendelea kuwatumikia wapiga kura wake.
Kutokana na hali hiyo January ambaye ni Mbunge wa Bumbuli, amewataka wananchi wake kuwapuuza watu wanaopita na kudai kuwa wanataka ubunge kwa kuwa yeye anatajwa katika kinyang’anyoro cha urais ndani ya CCM.
Kauli hiyo aliitoa juzi jimboni kwake Bumbuli, wilayani Lushoto mkoani Tanga katika mkutano wa hadhara ambapo alikuwa akizungumzia mafanikio na changamoto za utekelezaji wa ilani ya uchaguzi tangu alipochaguliwa mwaka 2010.
January alitumia mkutano huo kuwashukuru wapiga kura wake kwa kumchagua kuwa mbunge mwaka 2010 huku akisema kuwa kama si wao asingeweza kutajwa katika mbio za urais ndani ya CCM.
“Kutajwa si dhambi na kwa kuwa fomu za uchaguzi si sumu si dhambi kuchukua…. na kuingia katika kinyang’anyiro hicho.
“Hivi kuna kiu kubwa ya uongozi wa aina mpya na kuna watu wamemwona mtu na kumtaja yeye jambo ambalo si baya.
"Wapuuzeni watu wanaopita na kusema mimi sitaki ubunge eti kwa sababu natajwa kwenye urais.
"Wapuuzeni watu wanaopita na kusema mimi sitaki ubunge eti kwa sababu natajwa kwenye urais.
“Hayo ni maneno ya kilaghai na ya kukatisha tamaa na kichochezi msiyakubali. Kinyang’anyiro ni kama mchezo wa mpira kuna kushinda na kushindwa.
“Tukishindwa narudi hapa tuendeleze tuliyoyaanza, Rais Kikwete alijaribu mara ya kwanza kura hazikutimia akarudi jimboni hata pia Kigoda (Dk. Abdallah) naye alifanya hivyo ikashindikana akarudi kwenye ubunge,” alisema.
Akizungumzia hatua ya kufufua uzalishaji wa Kiwanda cha Chai Mponde, January alisema kuwa Serikali imeridhia kutoa Sh bilioni 4 ambazo ni gharama za kulipa madeni ya malimbikizo ya mishahara ya wafanyakazi.
Alisema mbali na hilo madeni ya malipo ya wakulima, gharama za ukarabati na mtaji wa kuanzia kuendesha shughuli za uzalishaji utaimarishwa.
January ambaye yupo katika ziara ya siku tano ya kutembelea jimbo lake, alisema Serikali ilituma wataalamu kufanya tathmini yenye lengo la kutambua gharama za ufufuaji wa kiwanda hicho kilichokuwa kikiendeshwa na Chama cha Wakulima wa Chai cha Usambara (Utega) na mwekezaji ambaye ni Lushoto Tea Company katika miaka ya mwanzo ya 2000.
Alisema kwa kuwa fedha hizo hazikuwa katika bajeti ya Serikali, ilibidi ofisi ya waziri mkuu kuomba kibali kutoka kwa rais ili kutoa fedha hizo.
“Mambo yote yako tayari. Kilichokuwa kinasubiriwa ni kibali ambacho kimekwisha kutolewa na Rais Kikwete. Hivi sasa ni Hazina ndiyo inayosubiriwa itoe fedha hizo kwa ajili ya kukarabati kiwanda na gharama nyingine,” alisema January.
Mgogoro huo ambao umeleta maumivu makali ya kiuchumi na kijamii kwa wakulima wapatao 4,000 walioko katika skimu tano za chai zilizopo katika eneo la Halmashauri ya Bumbuli, ulitatuliwa na Serikali na maamuzi hayo kutangazwa kwa wakulima na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana.
Baada ya tamko hilo ambalo amelieleza kuwa la kihistoria la kuchukua kiwanda kutoka kwa mwekezaji kukirejesha kwa wakulima, January alieleza kuwa Serikali ilianza harakati za kufufua kiwanda kwa kutuma timu ya wataalamu kufanya tathmini.
Wazee wambariki
Baada ya kumalizika kwa mkutano huo, wazee wa Bumbuli, walimpa baraka huku wakimuhakikishia kumwunga mkono katika harakati zake za kisiasa ndani ya Chama Cha Mapinduzi.
Waliotoa baraka hizo kwa niaba ya wazee ni Askofu Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili na Kirutheli Tanzania (KKKT) Lushoto, Amasia Mweta na Sheikh Yahya Mjata.
Ni dhahiri mpambano wa kuwania urais ndani ya CCM unazidi kunoga, ikiwa imebakia miezi michache kabla ya kupulizwa rasmi kipenga.
January Makamba ni mmoja wa makada kutoka CCM waliotangaza nia ya kuwania urais ndani ya CCM ambaye hivi karibuni aliandika kitabu kinachoeleza nia yake hiyo.
Katika kitabu hicho pamoja na mambo mengine kinaeleza mikakati ya mwanasiasa huyo kijana iwapo atapitishwa na chama chake ili kuwania na hatimaye kushika nafasi hiyo ya juu ya uongozi kitaifa.
Katika kitabu hicho chenye kurasa 196, January anasema rais ajaye lazima awe na tafakuri pana na nia ya kuendeleza nchi na si kuwa na kaulimbiu nyepesi za afya bure, elimu bure zisizo na ufafanuzi ili kuwahadaa wananchi.
Kitabu hicho kilichoandikwa na mchambuzi na mwandishi wa makala za siasa, Padri Privatus Karugendo kimebeba sera na mikakati yake kiundani ya kuiongoza nchi iwapo atapatiwa dhamana na CCM kugombea urais.
Katika kitabu hicho kinachoitwa, ‘Maswali na Majibu 40: Mazungumzo na January Makamba kuhusu Tanzania Mpya’, mwanasiasa huyo anasema uongozi hauishii kwa kauli za juu juu za kuongeza ajira, kuboresha elimu kwani kila mtu anaweza kuyasema hayo.
January, anasema katika tafakuri zake anaona rais ajaye anatakiwa kuzitambua kwa kina changamoto za nchi yake na kuwa na mikakati ya kuzitatua.
Kutokana na changamoto hizo, Janury anasema ni za kiuongozi na utatuzi wake unategemea kiongozi mwenyewe, hulka, mtazamo wake na usahihi wa uamuzi anaoufanya.
“Kuomba uongozi wa nchi si harakati binafsi na wafuasi wako kupata vyeo. Ni dhamana kubwa ya kujenga mustakabali wa nchi na kuwaunganisha Watanzania wote. Kwa hiyo, uamuzi wa kugombea lazima uupe heshima na nafasi inayolingana na dhamana yenyewe,”anasema January katika kitabu hicho.
Comments
Post a Comment